Eden Hazard: 'Nahisi hizi ni salamu za kuaga'
Eden Hazard amedokeza kuwa amemaliza safari yake na klabu ya Chelsea baada ya kufunga goli mbili zilizosaidia kuizamisha Arenal jana usiku.
Chelsea imeibuka na ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya Arsenal kwenye fainali ya kombe la Europa.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia Real Madrid na amesema kwa sasa "anasubiria klabu hizo (kukubaliana)."
"Nafikiri hii ni kwaheri ktoka kwangu, lakini kwenye mpira hauwezi kujua kitakachotokea."
Kocha wa Chelsea Maurizio Sarri amesema anaheshimu maamuzi ya Hazard.
- Chelsea yailaza Arsenal na kushinda kombe la ligi ya Europa
- Tetesi za soka Ulaya Alhamisi 30.05.2019
- Neymar avuliwa unahodha wa Brazil
"Najua anataka kuondoka na inanipasa niheshimu maamuzi yake," amesema kocha huyo raia wa Italia na kuongeza: "Ni mchezaji mzuri sana. Ilinichukua miezi miwili au mitatu kumuelewa, sasa namuelewa, japo ni mtukutu lakini ni mtu mwema."
Ikiwa mechi hiyo iliyopigwa katika jiji la Baku ndiyo ya mwisho kwa Hazard, basi itahitimisha safari yake ya miaka saba na miamba hiyo ya rangi ya samawati kutoka jiji la London.
Hazard, 28, alijiunga na Chelsea kutokea Lille ya Ufaransa kwa dau la pauni milioni 32.
Ameichezea Chelsea mechi 352 na amefunga jumla ya magoli 110.
Akizungumzia mustakabali wake, Hazard amesema: "Tutafikia uamuzi ndani ya siku chache zijazo - malengo yangu ya msngi kwa wakati huu yalikuwa kushinda kombe hili. Labda sasa ni muda wa kufikiria changamoto nyengine.
"Ndoto yangu ilikuwa kucheza Ligi ya Primia na nimefanya hivyo na moja ya klabu kubwa zaidi."
Hazard alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi ya Primia kwa msimu wa 2014/15, akifunga magoli 14 na kusaidia timu yake kunyakuwa ubingwa.
Msimu wa 2016/17 Chelsea pia walinyakuwa ubingwa wa Primia huku Hazard akifunga magoli 16.
Ubingwa wa sasa wa Europa ni wa pili kwa Hazard akiwa na Chelsea baada ya timu hiyo kushinda kombe hilo mwaka 2013.
Kiungo wa zamani wa Chelsea Cesc Fabregas amekiambia kituo cha runinga cha BT Sport kuwa: "Hazard akiwa na mpira mguuni unategemea kuna kitu kitatokea na wachezaji wote huwa wanapata nguvu mpya. Siwezi kusema kuwa atakuwa ndiye mchezaji bor zaidi katika historia ya klabu ya Chelsea, lakini ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa zaidi kuwahi kumpata.
0 comments: